Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ndugu. Wazo Mwang’onda ameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa jengo la utawala la Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma leo Juni 06, 2026.
Ujenzi wa jengo hilo utagharimu kiasi cha Sh Milioni 326 ambapo mpaka sasa tayari kiasi cha Sh Milioni 228 kimeshatumika.
Akizungumza mara baada ya kukagua na kuzindua ujenzi wa mradi huo, Kiongozi huyo wa Mbio za Mwenge, Ndugu Mwang'onda ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kupitia Wizara ya Nishati kwa namna inavyoendelea kuboresha na kusogeza huduma za umeme kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Chamwino ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi amesema ujenzi wa mradi wa jengo hilo ni muendelezo wa utekelezaji wa ahadi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya umeme.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaboresha mazingira ya kazi kwa watumishi wa TANESCO na kuongeza ufanisi wa huduma na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi lakini kuhamasisha wananchi kutumia nishati safi.
Mwenge wa Uhuru umekagua na kuzindua miradi saba ya maendeleo yenye thamani ya Sh Bilioni 3 kwenye Wilaya hiyo.









Hakuna maoni: