Paris, Ufaransa
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, amewasili leo nchini Ufaransa kwa ziara ya kikazi ya kushiriki na kuongoza vikao vya Bodi ya Global Partnership for Education (GPE), taasisi ya kimataifa inayojihusisha na maendeleo ya elimu duniani, ambako anahudumu kama Mwenyekiti wa Bodi.
Mhe. Kikwete alipokelewa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Charles de Gaulle na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Othman Yakubu, pamoja na watumishi wa Ubalozi wa Tanzania nchini humo.
Katika nafasi yake kama Mwenyekiti wa Bodi ya GPE, Mhe. Kikwete anaongoza juhudi za kimataifa zinazolenga kuimarisha upatikanaji wa elimu bora, jumuishi na yenye usawa kwa watoto katika nchi zinazoendelea. GPE ni ushirikiano wa kimataifa unaozileta pamoja serikali, mashirika ya maendeleo, sekta binafsi, asasi za kiraia na wadau wengine wa elimu ili kusaidia nchi zenye kipato cha chini na cha kati kuboresha mifumo yao ya elimu.
Kupitia ushirikiano huo, GPE hutoa msaada wa kifedha na kiufundi kwa nchi washirika ili kuongeza upatikanaji wa elimu ya msingi na sekondari, kuboresha ubora wa ufundishaji na ujifunzaji, kuimarisha usawa wa kijinsia katika elimu, pamoja na kuhakikisha watoto walio katika mazingira magumu wanapata fursa ya elimu.
Uongozi wa Mhe. Kikwete katika GPE umeendelea kuimarisha mchango wa Afrika na nchi zinazoendelea katika mijadala ya kimataifa kuhusu elimu, huku ukisisitiza umuhimu wa elimu kama nyenzo muhimu ya maendeleo endelevu na ustawi wa jamii.
Wakati wa ziara yake nchini Ufaransa, Mhe. Kikwete anatarajiwa kuongoza vikao mbalimbali vya Bodi ya GPE pamoja na kushiriki majadiliano ya kimkakati kuhusu mustakabali wa elimu duniani.







Hakuna maoni: