Na Mwandishi Wetu
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limekanusha taarifa zilizotolewa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (MWAUWASA) zikidai kuwa upungufu wa huduma ya maji jijini Mwanza ulisababishwa na kukosekana au kuyumba kwa umeme katika mitambo ya uzalishaji maji.
Katika taarifa kwa umma iliyotolewa Juni 14, 2026, TANESCO imesema madai hayo si ya kweli na kwamba uchunguzi wa kina uliofanywa katika mitambo ya uzalishaji maji ya Butimba na Capri Point umebaini kuwa hitilafu zilizosababisha changamoto ya upatikanaji wa maji zilikuwa ndani ya mfumo wa MWAUWASA na si kutokana na huduma ya umeme.
TANESCO imeeleza kuwa wakati wa uchunguzi huo, baadhi ya mitambo ilikaguliwa huku huduma ya umeme ikiendelea kupatikana katika viwango vya kawaida vya voltage vinavyokubalika kitaalamu, jambo lililothibitisha kuwa hakukuwa na hitilafu upande wa usambazaji wa umeme.
Aidha, shirika hilo limesema mapungufu yaliyobainika pamoja na mapendekezo ya kuyarekebisha yaliwasilishwa kwa uongozi wa MWAUWASA kupitia vikao vya pamoja na baadaye kwa njia ya barua rasmi ya Juni 11, 2026. Hata hivyo, baadhi ya mapendekezo hayo muhimu hayajatekelezwa hadi sasa.
Kutokana na hali hiyo, TANESCO imesisitiza kuwa hakukuwa na hitilafu yoyote ya umeme wala ukosefu wa huduma ya umeme katika kipindi husika ambacho kingeweza kuathiri uzalishaji na usambazaji wa maji kama ilivyodaiwa.
Shirika hilo pia limezitaka taasisi zinazotoa huduma kwa umma kutoa taarifa sahihi na kushughulikia changamoto zinapojitokeza badala ya kuelekeza lawama kwa taasisi nyingine bila ushahidi wa kutosha.
TANESCO imesema itaendelea kushirikiana na taasisi mbalimbali zinazotoa huduma muhimu kwa wananchi ili kuhakikisha huduma hizo zinapatikana kwa uhakika, ufanisi na viwango vinavyokubalika.


Hakuna maoni: