TEMEKE YAADHIMISHA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA, BOYS INITIATIVE YAPAZA SAUTI YA MTOTO WA KIUME

Na Mwandishi Wetu, 

Dar es Salaam. 

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Wilaya ya Temeke, Lawama Mikidadi, amesema Maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika ni fursa muhimu ya kuikumbusha jamii wajibu wake wa kulinda na kutetea haki za msingi za watoto.

Akizungumza katika maadhimisho hayo yaliyofanyika leo wilayani Temeke, Mikidadi amesema siku hiyo huadhimishwa kila mwaka Juni 16, lakini kwa mwaka huu wilaya hiyo imeanza maadhimisho mapema kwa kuwafikia watoto na jamii kwa ujumla.

Amesema licha ya jitihada mbalimbali zinazoendelea kufanywa, vitendo vya ukatili wa kijinsia dhidi ya watoto bado vipo katika baadhi ya maeneo, hivyo wilaya imeendelea kuweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha vitendo hivyo vinatokomezwa kabisa.

Aidha, amewataka wazazi na walezi kutimiza wajibu wao wa kuwalinda watoto na kuepuka kuwa sehemu ya vitendo vya ukatili vinavyoweza kuhatarisha ustawi na maendeleo yao.

Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Polisi kutoka Dawati la Jinsia na Watoto Wilaya ya Temeke, Brandina Ndunguru, ametoa elimu kwa wanafunzi waliohudhuria maadhimisho hayo akiwataka kujiepusha na vishawishi mbalimbali vinavyoweza kusababisha ukatili wa kijinsia.

Amesema watoto wanapaswa kuwa waangalifu dhidi ya watu wasiowafahamu wanaowapa zawadi au kuwashawishi kwa namna mbalimbali, huku akiwahimiza kutoa taarifa kwa wazazi, walezi au watu wanaowaamini wanapoona viashiria vya ukatili.

Ndunguru amesema watoto wanapaswa kufahamu mipaka ya usalama wao na kutoa taarifa mara moja endapo mtu yeyote atajaribu kuwagusa sehemu zisizofaa au kutumia lugha isiyofaa dhidi yao.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali limeendelea kutoa elimu kwa jamii na familia kuhusu masuala ya ukatili wa kijinsia, huku akibainisha kuwa baadhi ya watu wamekuwa wakifanya vitendo vya ukatili bila kutambua kuwa ni makosa ya kisheria na kijamii.

Pia amesisitiza kuwa mtoto hapaswi kutumwa usiku kwenda maeneo ya mbali, wala kulala na wageni, akieleza kuwa mazingira hayo yanaweza kuongeza hatari ya kufanyiwa ukatili.

"Mtoto anapaswa kulindwa, kusikilizwa na kupewa nafasi ya kueleza changamoto zake. Wazazi wajenge urafiki na watoto wao ili waweze kuwasaidia kwa karibu zaidi," amesema.

Naye Mratibu wa Maendeleo ya Mtoto wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Sweetbertha Pascal, amesema maadhimisho hayo yameandaliwa kwa kutambua umuhimu wa mtoto katika kujenga jamii bora na taifa imara.

Amesema Halmashauri ya Temeke imeendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia shule mbalimbali na mitaa yote 42 ya manispaa hiyo, ambapo maafisa ustawi wa jamii wamekuwa wakitoa elimu kuhusu malezi bora na kupinga ukatili wa kijinsia.

Kwa mujibu wake, shule sita zimeshiriki katika maadhimisho ya mwaka huu, ambapo wanafunzi wamepatiwa elimu mbalimbali pamoja na kushiriki michezo na shughuli nyingine za kijamii.

Maadhimisho ya mwaka huu yameongozwa na kaulimbiu isemayo, "Mtoto ni Malezi, Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara."

Kwa upande mwingine, Mkurugenzi na Mwanzilishi wa Taasisi ya Boys Initiative Tanzania, Dianarose Rweyemamu, amesema taasisi hiyo imejikita katika kutetea na kupaza sauti ya mtoto wa kiume ambaye mara nyingi amekuwa hasikiki katika mijadala mingi ya maendeleo ya watoto.

Amesema ni muhimu kwa serikali, wadau wa maendeleo na jamii kwa ujumla kuzingatia changamoto zinazowakabili watoto wa kiume sambamba na jitihada zinazofanyika kwa watoto wa kike.

"Tunataka kuona agenda ya mtoto wa kiume inapewa kipaumbele sawa na mtoto wa kike ili kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa za maendeleo na ulinzi," amesema.

Wakizungumza kwa niaba ya watoto walioshiriki maadhimisho hayo, Edwin John amesema elimu waliyoipata imewasaidia kuelewa haki zao pamoja na namna ya kujilinda dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia. Amesema watoto wanapaswa kuwa na ujasiri wa kutoa taarifa wanapoona au kufanyiwa vitendo visivyofaa ili waweze kupata msaada kwa wakati.

Naye Asha Juma amesema maadhimisho hayo yamewapa watoto nafasi ya kujifunza mambo muhimu kuhusu usalama wao na wajibu wa wazazi katika malezi bora. Amesema watoto wanapaswa kusikiliza ushauri wa wazazi na walezi wao na kuepuka kushawishiwa na watu wasiowafahamu ili kujikinga na vitendo vya ukatili.

Maadhimisho hayo yamekusanya wanafunzi, walimu, viongozi wa serikali, wadau wa maendeleo ya watoto pamoja na wananchi wa Wilaya ya Temeke kwa lengo la kuhamasisha jamii kuendelea kulinda haki na ustawi wa watoto.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.