TANZANIA NA COMORO KUWEKA HISTORIA MPYA KWENYE USAFIRI WA NDEGE

Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) umeandika historia mpya katika sekta ya usafiri wa anga baada ya kupokea rasmi safari za ndege za kampuni ya Royal Air zinazounganisha moja kwa moja Tanzania na Comoro.

Uzinduzi wa safari hizo unatarajiwa kuimarisha usafiri wa abiria, usafirishaji wa mizigo na kukuza biashara kati ya mataifa hayo mawili jirani ambayo kwa muda mrefu yamekuwa na uhusiano wa karibu wa kiuchumi na kijamii.

Akizungumza Leo wakati wa hafla ya uzinduzi wa safari hiyo Mkurugenzi wa Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere, Bertha Bankwa, alisema kuanza kwa huduma za Royal Air ni mafanikio makubwa kwa sekta ya usafiri wa anga nchini kwani kunaongeza idadi ya mashirika ya ndege yanayohudumia njia ya Tanzania na Comoro.

Amesema ndege hiyo itakuwa ikifanya safari mara nne kwa wiki, siku za Jumatatu, Jumatano, Ijumaa na Jumapili. Alibainisha kuwa safari za Ijumaa zitakuwa na utaratibu maalum ambapo ndege itawasili ikiwa na abiria na kurejea Comoro ikiwa imebeba mizigo.

Bankwa amesema ujio wa Royal Air utaongeza ushindani chanya katika soko la usafiri wa anga na kusaidia kuongeza mapato ya kiwanja kupitia ongezeko la idadi ya abiria na mizigo inayosafirishwa. 

Ameeleza kuwa tayari njia hiyo inahudumiwa na mashirika mengine ya ndege, yakiwemo Air Tanzania na Precision Air, jambo linaloonyesha kuwepo kwa mahitaji makubwa ya usafiri kati ya Tanzania na Comoro.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.