Na Beda Msimbe,
TBN – Moscow
Tanzania na Urusi zipo katika hatua za mwisho za majadiliano kuhusu mfumo wa malipo ya biashara kwa lengo la kuimarisha biashara na uwekezaji kati ya mataifa hayo mawili.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wanaoambatana na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika ziara yake ya kitaifa nchini Urusi.
Profesa Mkumbo amesema nchi hizo zinatarajia kusaini hati za makubaliano kabla ya kumalizika kwa ziara hiyo, hatua itakayorahisisha miamala ya kibiashara na kuongeza ushirikiano wa kiuchumi.
Amesema kwa sasa kiwango cha biashara kati ya Tanzania na Urusi kinafikia dola za Marekani milioni 200, na makubaliano hayo yatafungua fursa zaidi za biashara na uwekezaji.
Aidha, amefafanua kuwa mfumo huo mpya wa malipo utahusisha matumizi ya Shilingi ya Tanzania, jambo litakalopunguza changamoto za miamala ya kimataifa.
Profesa Mkumbo amesema Urusi, ambayo ilishiriki katika harakati za ukombozi wa kisiasa wa Afrika, sasa inaendelea kuwa mshirika muhimu katika ukombozi wa kiuchumi kupitia sekta za kilimo, uchakataji wa mazao, uzalishaji wa mbegu bora na madini.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo utakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayotarajiwa kuanza kutumika mwezi Julai mwaka huu.
Kwa upande mwingine, amesema moja ya manufaa makubwa ya ziara hiyo ni kuendelea kwa mazungumzo yatakayowezesha ujenzi wa Reli ya Kusini kupitia mfumo wa ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi (PPP).
Pia amesema Tanzania na Urusi zipo katika hatua za mwisho za makubaliano yatakayowezesha Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Moscow, hatua inayotarajiwa kukuza utalii, biashara na uwekezaji kati ya nchi hizo mbili.



Hakuna maoni: