Imeelezwa kwamba mbolea za asili na mbolea za viwandani zote zinafaa shambani tofauti ni kwamba mbolea za asili huchelewa kuleta matokeo(kwani hufanya kazi polepole) ukilinganisha na zile za viwandani.
Hayo yamebainishwa na msimamizi wa ofisi ya Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) Revocatus Rwegoshora hivi karibuni akitoa elimu kwa watembeleaji wa Banda katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.
Amesema, mbolea za asili huchukua muda mrefu kuonesha matokeo shambani ikilinganishwa na za viwandani jambo linaloenda sambamba na wakulima wengi kutumia kiasi kidogo au virutubisho vyake kutodhibitishwa tofauti na zile za viwandani.
Sambamba na hilo, ilielezwa kuwa mbolea za asili hazina viwango vya virutubisho vinavyolingana kwani hutegemea aina ya malighafi iliyotumika, chakula walichokula wanyama/mifugo, muda na njia ya utengenezaji au uozeshaji pamoja mazingira kama vile joto au unyevu.
Amesema mbolea za viwandani zina virutubisho vilivyobainishwa kwa mfano NPK 15:9:20 ambapo mkulima akiweka mbolea hiyo anakuwa na uhakika kuwa virutubisho vilivyowekwa shambani vina kiwango kinachohitajika.
Aidha, amewasihi wakulima kuzingatia taratibu na hatua za kufuata katika kuandaa mbolea zinazotokana na mazao na mifugo ikiwemo samadi na mboji ili kuhakikisha wanapata mbolea bora.
Amewasili kuchimba shimo maalum ambalo litatumika kutunzia samadi/mboji hiyo kuhakikisha virutubisho havitawanyiki na kupotea.
Mamlaka inatoa wito kwa wananchi kutembelea banda hilo ili kupata huduma zinazotolewa ikiwa ni pamoja na kusajili na kuhuisha taarifa za mkulima kwenye mfumo wa pembejeo za ruzuku.






Hakuna maoni: