Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa agenda ya nishati safi ya kupikia, ambapo upatikanaji wa huduma hiyo umeongezeka kutoka asilimia 6.9 mwaka 2021 hadi asilimia 28.6 mwaka 2025.
Amesema mafanikio hayo yametokana na uongozi thabiti wa Serikali, ushirikiano wa wadau wa maendeleo, sekta binafsi na kuongezeka kwa uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya nishati safi.
Akifungua rasmi Mkutano wa Wadau wa Nishati Safi ya Kupikia 2026 uliofanyika Arusha leo Juni 10,2026 Mhe. Salome amesema Serikali imejipanga kufikia lengo la asilimia 80 ya Watanzania kutumia nishati safi ya kupikia ifikapo 2034 kupitia utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia wa mwaka 2024–2034.
‘Miradi mbalimbali imechangia mafanikio hayo ikiwemo usambazaji wa mitungi 452,445 ya LPG, majiko banifu 200,000, pamoja na utekelezaji wa mradi wa CookFund unaofadhiliwa na Umoja wa Ulaya kupitia UNCDF, ambao umewezesha kaya zaidi ya 634,000 kupata huduma za nishati safi ya kupikia katika mikoa mbalimbali nchini’.
Pia amewataka wadau wote kuendelea kushirikiana ili kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata nishati safi, salama na nafuu ya kupikia, huku akisisitiza kuwa agenda hiyo ni muhimu kwa afya, mazingira, uchumi wa kaya na maendeleo endelevu ya Taifa.
Mkutano huo ulioandaliwa na UNCDF ukiwa na kwa lengo la kujadili maendeleo, fursa na mikakati ya kuharakisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini Tanzania.





Hakuna maoni: