OFISI YA WAZIRI MKUU YAHIMIZA USHIRIKIANO KWA MAENDELEO YA TAIFA

DKT. MUNISI: UMOJA NA USHIRIKIANO NI NGUZO YA MAENDELEO YA TAIFA

DAR ES SALAAM. 

Naibu Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Eveline Munisi, amesema mafanikio ya maendeleo nchini yanategemea uwepo wa mahusiano imara kati ya wananchi, taasisi na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari katika Maonesho ya 50 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba) yaliyofanyika Julai 5, 2026, Dkt. Munisi alisema Serikali inaendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi za kidini, asasi za kiraia, vyama vya siasa pamoja na wadau wengine kwa lengo la kuendeleza amani, mshikamano na umoja wa kitaifa.

Alieleza kuwa jamii inayoshirikiana kwa karibu huweka msingi bora wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku akiwataka Watanzania kuendelea kudumisha utamaduni wa kushirikiana kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.

Kwa upande wa ajira na maendeleo ya rasilimali watu, Dkt. Munisi alisema Serikali inaendelea kutekeleza programu mbalimbali za kuwajengea vijana ujuzi unaohitajika katika soko la ajira, hatua ambayo itaiwezesha Tanzania kuwa na wataalamu wa kutosha kutoka ndani ya nchi na kupunguza utegemezi wa wataalamu wa kigeni.

Aidha, aliwahamasisha wananchi wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika katika banda la Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Ajira na Mahusiano) ili kujifunza kuhusu huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na ofisi hiyo pamoja na taasisi zilizo chini yake.

Hakuna maoni:

Inaendeshwa na Blogger.